Call for Interview

Placements

Visitors Counter

»Today   1521               
»Week   1521               
»Month   29282               
==============
»Total  23379668        

TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA SEKRETARIETI YA AJIRA ILIYOWASILISHWA NA KATIBU WA SEKRETARIETI HIYO.

November 5, 2017


Mheshimiwa Waziri,

Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii adhimu kwa niaba ya jamii nzima ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kukupongeza kwa kuaminiwa na hatimaye kuteuliwa na Mheshimiwa Rais, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Nafasi ambayo ni nyeti na yenye Majukumu makubwa. Hongera sana.

Pili, nichukue fursa hii kukushukuru kwa ujio wako na kukukaribisha Sekretarieti ya Ajira, ikiwa ni mara yako ya kwanza kuitembelea Taasisi yako ukiwa Waziri mwenye dhamana. Kwa mujibu wa ratiba tuliyoipokea tunaamini kwa taasisi zilizo chini ya Utumishi, hii ni taasisi yako ya kwanza kuitembelea. Mheshimiwa Waziri karibu sana na tunashukuru kwa kutupa heshima hiyo.

Mheshimiwa Waziri,

Ninaamini ziara hii itaendelea kukuwezesha kuzifahamu taasisi zako vizuri zaidi pamoja na kufahamiana na Watendaji, utendaji wetu wa kazi, na kujua changamoto tunazokabiliana nazo. Aidha, sisi Sekretarieti ya Ajira ambao tumepewa jukumu la kutafuta rasilimaliwatu inayopaswa kuingia Serikalini, tunaahidi kukupatia ushirikiano wa hali ya juu ili kukuwezesha kutekeleza majukumu yako. Pamoja na kukuwezesha kutekeleza ilani ya chama kilichopo madarakani.

Mheshimiwa Waziri,

Baada ya kusema hayo naomba nianze kwa kuelezea historia fupi ya Sekretarieti ya Ajira.

UTANGULIZI

Mheshimiwa Waziri,

Chimbuko la Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetokana na Sheria ya Utumishi wa Umma Na.8 ya 2002 hususan,Kupitia Marekebisho ya Sheria hiyo Na.18 ya 2007 pamoja na Tamko la Sera ya Menejimenti na Ajira toleo  Na. 2 la 2008 ambayo ilielekeza kuundwa kwa chombo maalum(huru) kitakachoshughulikia masuala ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Mheshimiwa Waziri,

Kufuatia marekebisho hayo ya Sheria, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilianza kazi tarehe 24 Juni, 2009 na ilianza kutekeleza majukumu yake rasmi tarehe 01Machi, 2010. Aidha, usaili wa kwanza kuendeshwa na chombo hiki ulifanyika mwezi Juni, 2010.Sambamba na utekelezaji huo wa majukumu lakini pia Chombo hiki kimekuwa chini ya Uongozi wa Bodi mbili na Bodi mpya ya tatu ni hii iliyozinduliwa hivi karibuni chini ya Wenyekiti wa Bibi Rose M. Lugembe ambaye yupo pamoja nasi leo na Wajumbe wake watano ambao ni Bw. Mbarak M. Abdulwakili (Makamu Mwenyekiti) yeye anatoka upande wa pili wa Muungano (Zanzibar), Bw.  Fanuel E. Mbonde (Mjumbe), Bibi Tamika L. Mwakahesya (Mjumbe) Bw. Aloyce L. Msigwa (Mjumbe) pamoja na  Bw. John N. Joel (Mjumbe).

Mheshimiwa Waziri,

Naamini sitakuwa nimetenda haki kama sitatumia fursa na hadhara hii kumshukuru kwa dhati kabisa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki kwa kuwa tunaamini ana mchango mkubwa kwetu hadi kufikia hapa tulipo leo. Tunamshukuru sana na kumtakia kila la kheri katika majukumu yake mapya, akiwa Waziri mwenye dhamana ya Madini.

 LENGO LA KUANZISHWA  KWA SEKRETARIETI YA AJIRA

Mheshimiwa Waziri,

Chombo hiki kiliundwa kwa lengo kuu la kuendesha mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma ili kuziwezesha mamlaka za Ajira kupata nafasi ya kutekeleza majukumu yake ya msingi kama yalivyoainishwa katika Hati Rasmi (Instruments) zilizoanzisha Taasisi hizo.

Sekretarieti ya Ajira imekuwa ikiendesha mchakato wa ajira  kwa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni pamoja na Taratibu kwa kushirikiana na Wizara, Idara,Wakala wa Serikali, Taasisi za Umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuweza kufanikisha upatikanaji wa Watumishi wa Umma wenye sifa, ujuzi, uzoefu, na maadili mema.

Mheshimiwa Waziri, 

Aidha, uanzishwaji wa Sekretarieti ya Ajira ulilenga kuondoa changamoto za awali ambazo ziliikabili eneo la ajira katika Utumishi wa Umma ambazo ni:-

Kukosekana kwa taarifa nyingi na muhimu za ajira kwa wakati pale zinapohitajika kutokana na taarifa hizo kusambaa kwa waajiri mbalimbali.

Kutozingatiwa kwa sifa zinazohitajika kulingana mahitaji ya kazi (Lack of Meritocracy) wakati wa kuajiri.

Kukosekana kwa waombaji wenye sifa kwenye baadhi ya maeneo nchini.

Kukosekana kwa maadili wakati wa kushughulikia mchakato wa ajira.

Udhaifu katika uelewa wa kuendesha na kusimamia mchakato wa ajira ambapo maarifa, ujuzi na sifa havikuzingatiwa.

Serikali kutenga kiwango kikubwa cha bajeti kwenye ajira kwa nafasi ambazo hazijazwi na waajiri kwenye mwaka husika.

Serikali kutumia kiwango kikubwa cha fedha kwa ajili ya gharama za matangazo ya kazi yanayofanywa na kila mwajiri mmoja mmoja.

Baadhi ya Waajiri kutolichukulia zoezi la ajira kama muhimu kwa taasisi zao, na kutozingatia kikamilifu majukumu yao ya msingi.

Kuibuka kwa masuala ya ukabila, rushwa na upendeleo katika kuajiri watumishi, hivyo kutishia dhana ya utaifa.

Baadhi ya Waajiri kukosa watumishi kutokana na tabia ya baadhi ya Waombaji kazi kuchagua mikoa ya kufanyia kazi au taasisi za kufanyia kazi.  Aidha, katika kipindi hicho waajiri wengi walipata hasara kutokana na waajiriwa kuomba maeneo mengi wakati amesharipoti kwa mwajiri na pengine kuwa ameshalipwa stahili zake. Malipo ambayo mtumishi anapoondoka hayakurejeshwa na hivyo kulazimika kuajiri tena na kutumia gharama tena za kulipa mtumishi mpya.

MAJUKUMU YA SEKRETARIETI YA AJIRA

Mheshimiwa Waziri,

Kutokana na Changamoto nilizozitaja Sekretarieti ya Ajira ilianzishwa kisheria ili kukabiliana na changamoto hizo za mifumo ya awali.Taasisi hiii imepewa majukumu ya kisheria yafuatayo:

Kutafuta wataalam wenye ujuzi maalum na kuandaa mfumo wa   kuhifadhi taarifa (kanzidata) za wataalam hao ili kurahisisha utaratibu wa kuwaajiri pindi wanapohitajika;

Kuandaa orodha ya wahitimu wa Vyuo Vikuu na Wataalam Weledi (Professionals) kwa madhumuni ya kurahisisha rejea na ujazaji wa nafasi wazi za ajira katika Utumishi wa Umma;

Kutangaza nafasi wazi za kazi zinazotokea katika Utumishi wa Umma;

Kuhusisha wataalam maalum (Appropriate experts) kwa ajili ya kufanya usaili kulingana na mahitaji;

Kutoa ushauri kwa Waajiri kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na ajira.

MUUNDO WA TAASISI

Mheshimiwa Waziri,

Sekretarieti ya Ajira kimuundo ina ngazi mbili;

Wajumbe wa Sekretarieti ya Ajira (Bodi);

Watendaji.

Taasisi hii inaongozwa na Mwenyekiti na Wajumbe watano na kufanya jumla yao kuwa sita. Pia, chini yao kuna Watendaji ambao wanaongozwa na Katibu akiwa na Idara na Vitengo vifuatavyo;

Idara ya Ajira, hii inaongozwa na Naibu Katibu, ambapo Idara hii ina sehemu mbili, zinazoongozwa na Katibu Wasaidizi wawili.

Idara ya Utawala na uendelezaji Rasilimaliwatu inaongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Uendelezaji wa Rasilimaliwatu.

Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, kinaongozwa na Naibu Katibu.

Kitengo cha Udhibiti wa Ubora, kinaongozwa na Naibu Katibu.

Kitengo cha Uhasibu na Fedha, kinaongozwa na Mhasibu Mkuu.

Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani, kinaongozwa na Afisa Ukaguzi Mkuu wa Ndani.

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, kinaongozwa na Afisa Habari Mkuu.

Kitengo cha Huduma za Sheria, kinaongozwa na Afisa Sheria Mkuu.

Kitengo cha Ununuzi na Ugavi, kinaongozwa na Afisa Ununuzi Mkuu.

Kitengo cha Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji, kinaongozwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo.

UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU

Uendeshaji Mchakato wa Ajira.

Mheshimiwa Waziri,

Sekretarieti ya Ajira inaendesha Mchakato wa Ajira kupitia hatua zifuatazo;

Mamlaka za Ajira kutenga katika bajeti yake mahitaji ya watumishi na kukubaliana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-MUUB) juu ya nafasi mpya na za mbadala.

Mamlaka za Ajira kuomba kibali cha Ajira toka OR-MUUB.

Sekretarieti ya Ajira kupokea vibali vya ajira toka mamlaka za Ajira na kutangaza, kusaili, kuchagua na kuwapeleka (post/make placement) kwenye mamlaka za ajira zilizoleta vibali hivyo ili zikamilishe taratibu za ajira kwa wahusika.

Alama za Ufaulu

Alama za ufaulu hutegemea na nafasi iliyotangazwa kama Kanuni ya 16 (1) (a – c)

Maafisa Watendaji Wakuu wa Taasisi za umma alama 60

Wataaluma katika taasisi za elimu ya juu alama 70

Maafisa na wasio maafisa  alama 50

Masuala yanayozingatiwa wakati wa kuwapangia vituo wasailiwa Waliofaulu Usaili kwa Waajiri ni pamoja na;

Ufaulu wao na nafasi zinazohitajika kulingana na kibali kilichowasiliswa pamoja na sifa zilizoainishwa.

Kipaumbele kwa walemavu kwa mujibu wa Kanuni ya 17 (2) kama inavyoelekeza pindi msailiwa akiweza kufikia ufaulu sawa na wengine.

Kutoa kipaumbele kwa wanawake pale wanapofungana kwa ufaulu sawa na wanaume.

Endapo wasailiwa waliofaulu na kufungana maksi ni wa jinsia moja mwenye umri mkubwa atapewa kipaumbele.

Wasailiwa waliopo kwenye kanzidata hupangiwa kazi kwa kuzingatia ufaulu wao na baada ya kuridhia kwenda kwa mwajiri husika.

3.0.  KUKASIMU KWA MAJUKUMU YA UENDESHAJI WA MCHAKATO WA AJIRA

Mheshimiwa Waziri,

            Kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 yam mwaka 2012 yaliyofanywa kupitia Sheria Na. 2 ya mwaka 2013.  Katibu kupitia Tangazo la Serikali Na. 70 la tarehe 14/3/2014 alikasimu kazi na majukumu ya Sekretarieti ya Ajira katika kuendesha mchakato wa Ajira kama ifuatavyo:-

Kwa Watendaji Wakuu wa Vyuo Vikuu 11 vya Umma kwa kada za Wanataaluma;

Kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa alikasimisha kada 22 kwa Watumishi wa kada za masharti ya kawaida, ambapo kila wakiendesha mchakato Katibu wa Sekretarieti hutuma mwakilishi ili kuhakikisha taratibu na sifa nyingine za msingi zinazingatiwa wakati wa mchakato.

Udhibiti na Ubora

Mheshimiwa Waziri,

Sekretarieti ya Ajira katika kuhakikisha Serikali inapata Watumishi wenye sifa,  ujuzi na maadili mema  ambao wana uwezo wa  kuiwezesha Serikali kutimiza malengo yake kwa ufanisi imekuwa na Kitengo kinachosimamia jukumu zima la udhibiti wa ubora wakati wa kuendesha mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma  kwa mujibu wa Sheria.

Kuhusisha Wataalam Maalum (Appropriate experts) kwa ajili ya kushirikiana nao katika kutunga maswali, kusahihisha, kuhakiki vyeti na taarifa za waombaji wa fursa za Ajira serikalini, kusimamia usaili kulingana na mahitaji pamoja na kutoa ushauri kwa Waajiri kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na mchakato wa  ajira ili kuhakikisha haki, usawa, uwazi; Sheria, kanuni na taratibu zinazingatiwa.

Baadhi ya taasisi na Mamlaka ambazo hushirikiana nazo katika zoezi la uhakiki ni pamoja na;

Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA);

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU)

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE)

Mamlaka ya Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA)

Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA)

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)

Chuo cha Usafirishaji (NIT)

Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC)

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)

Chuo cha Wanyamapori (MWEKA)

Vyuo Vikuu vya Umma na binafsi nchini.

MAFANIKIO

Mheshimiwa Waziri,

Sekretarieti ya Ajira imeweza kutekeleza majukumu yaliyoainishwa kisheria kwa mafanikio makubwa, Pamoja na mafanikio lakini pia tumeweza kukabiliana na changamoto kadhaa ambazo nitazitaja muda si mrefu.

Katika utekelezaji wa majukumu ya Sekretarieti ya Ajira   imeweza kupata mafanikio yafuatayo:

Tangu kuanzishwa kwa Sekretarieti ya Ajira hadi kufikia mwezi Oktoba maombi yaliyopokelewa ni 472,516.

Kuanzia mwaka 2010 tulipoanza kutekeleza majukumu yetu kwa mara ya kwanza hadi Oktoba, 2017 Sekretarieti ya Ajira imeshawapangia vituo vya kazi zaidi ya waombaji kazi 23,676.

Katika kutekeleza maamuzi ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhamishia shughuli zake Makao Makuu ya Serikali Dodoma tayari Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imepata uwanja wake eneo jirani na Ofisi za sasa la Wizara ya Fedha na Mipango kwenye eneo linalojulikana kwa jina  la NCC Link Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Ofisi zake. Naamini miaka michache ijayo tutaondokana na gharama kubwa la pango.

Tumeweza kufungua Ofisi eneo la Shangani Zanzibar na tayari Ofisi hiyo kwa sasa ina Watumishi Watatu na inafanya kazi. Ofisi hii ilifunguliwa mahsusi kwa ajili ya kurahisisha uendeshaji wa Ajira kwa Watumishi wa Taasisi za Muungano na wakati mwingine hata wale wa Taasisi zisizo za Muungano.

Baada ya Ajira kufunguliwa katika mwaka wa 2017/18 tumepokea vibali vya Ajira 292 vyenye jumla ya idadi ya nafasi 2,611 na mpaka kufikia Septemba, 2017 idadi ya waombaji 185 wamekwisha kupangiwa vituo vya kazi. Tuna vibali vingi ambavyo vipo kwenye hatua mbalimbali, ambapo baadhi ya usaili tutaendelea nao kwa juma lote linaloanzia leo tarehe 16 Oktoba, 2017. Baadhi ya taasisi ambazo tunaendesha usaili kwa juma hili ni MHN, MOI, TFS, GCLA,LGTI na EASTC pamoja na kuwapangia vituo vya kazi wasailiwa waliofaulu usaili.

Sekretarieti ya Ajira imepokea na kujumuisha taarifa za Maafisa Waandamizi na wenye taaluma/ujuzi maalum katika Utumishi wa Umma kwa lengo la kutengeneza kanzidata. Kanzidata hii tunaamini itarahisisha michakato ya kujaza nafasi wazi za juu katika Utumishi wa Umma.   Mpaka kufikia mwezi Juni, 2017 tumepokea orodha ya Maafisa kutoka Wizara tano, Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya jumla zipatazo 39, Wakala tatu, Chuo Kikuu kimoja na Taasisi tisa zimepokelewa. Taarifa hizo zinafanya jumla ya Watumishi Waandamizi 1,091 kupatikana taarifa zao pindi zitakapohitajika.

Tumeweza kwa kiasi kikubwa kudhibiti na kupunguza matumizi ya vyeti vya kughushi katika mchakato wa ajira Serikalini, Kutokana na uhakiki tunaofanya tangu  Ofisi hii ilipoanzishwa hadi kufikia sasa   tuna orodha ya majina ya waombaji kazi walio bainika kutumia vyeti vya kughushi 1,996 wakati wa kuomba kazi Serikalini, ambapo kati ya vyeti hivyo vya kughushi vya Sekondari ni  1,275, Leseni za Udereva 2, vyeti vya mafunzo ya Udereva vya VETA na NIT ni 558, vyeti vya kuzaliwa 86 na vyeti vya taasisi mbalimbali 75.

Tumeweza kuhifadhi na kutunza orodha ya majina ya waombaji kazi ambao wamepoteza, kuunguza au kuharibikiwa na vyeti vya sekondari, yaani kidato cha Nne (CSEE)na kidato cha Sita (ACSEE) kutoka Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA). Orodha hiyo ipo kwenye mtandao, mhusika anaweza kuiona endapo atakumbuka index namba yake.

Sekretarieti ya Ajira imejenga mifumo mbalimbali ya TEHAMA kwa lengo kurahisisha upashanaji habari, kuboresha mchakato wa Ajira na kurahisisha utendaji kazi wa Watumishi. Mifumo iliyosimikwa ni pamoja na Tovuti ya Sekretarieti ya Ajira, mfumo wa ujumbe mfupi wa simu za kiganjani (bulk sms), mfumo wa kupokea maombi ya kazi (recruitment portal) na mfumo wa barua pepe za kiofisi.

Jumla ya Watumishi nane (8) wamefanya mafunzo ikiwa  watumishi wanne (4) wako katika mafunzo ya muda mrefu kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili katika fani za TEHAMA (1), na Rasilimali watu (3) na watumishi wanne (4) wamehudhuria mafunzo ya muda mfupi nchini India kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kitaaluma ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wao; Nichukue fursa hii kuishukuru Ofisi yako pamoja na nchi rafiki kwa kutupa fursa ya kusomesha Watumishi wetu kwa gharama za nchi hizo.

Sektretarieti ya Ajira imeweza kutembelea na kubadilishana uzoefu na Wadau wake mbalimbali ikiwemo Mikoa ya Tanzania Bara, Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar, Baadhi ya Wizara na taasisi za Dar es Salaam, na sasa tumeanza ratiba ya kutembelea Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania Bara.Muda wowote kuanzia sasa tutaanza na Chuo cha Utumishi wa Umma kwenye Matawi yake yote na ziara nyingine nyingi zitafanyika kati ya Oktoba mwishoni na Novemba kipindi ambacho Vyuo vingi vitakuwa vimefunguliwa.

Sekretarieti ya Ajira imeweza kuendesha zoezi la usaili katika Mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar ili kusogeza huduma karibu na wadau pamoja na kuwapunguzia gharama wasailiwa za kusafiri hadi Dar es Salaam. Zoezi la mwisho tumelifanya mwezi wa Septemba ambapo tuliendesha usaili wa mchujo katika kanda 10 za nchi yetu ikiwemo Zanzibar.

Sekretarieti ya Ajira imeendelea kuimarisha mawasiliano na wadau wake kwa kutumia mifumo ya TEHAMA. Hadi kufikia 16 Oktoba, 2017 tovuti ya Sekretarieti ya Ajira (www.ajira.go.tz) imeshatembelewa zaidi ya mara milioni 22,575,840. Tangu mwezi huu wa Oktoba uanze kwa siku 16 tu tovuti yetu imetembelewa mara 513,622 na kufanya wastani kwa siku watu 32,101. Sambamba na hilo katika kuhakikisha wadau wetu wanapata taarifa sahihi tumeweza kuandaa vipeperushi mbalimbali na kuvisambaza kwa wadau wetu wakiwemo Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na wadau wengine. Pia, tumekuwa tukitumia Magazeti, Radio na Televisheni kutoa habari. Pamoja na  simu za kiganjani kwa ajili ya kutoa ufafanuzi na kupokea mrejesho wa wadau ambazo hupatikana muda wote wa kazi (+255 784 398 259/ 0687624975). Pia imefungua ukurasa katika mitandao ya kijamii ya "facebook" (www.facebook.com/sekretarieti), twitter (https://twitter.com/psrsajira) na youtube (https://www.youtube.com/Sekretarieti ya Ajira). Lengo la kuanzishwa kwa kurasa mbalimbali katika mitandao ya kijamii ni pamoja na kupanua wigo wa mawasiliano kwa wadau mbalimbali.

Mfumo wa kuhifadhi taarifa (kanzidata) za wataalam ili kurahisisha utaratibu wa kuwaajiri pindi wanapohitajika umeanzishwa na kutumika. Kutokana na matumizi ya kanzidata, Inachukua muda mfupi sana kuweza kupeleka watumishi kwa waajiri (chini ya wiki moja) baada ya kupata kibali cha ajira toka kwa mwajiri ikilinganishwa na kuanza mchakato upya ambao huchukua siku 52 au zaidi hadi kukamilika. Vilevile, imepunguza gharama za kuendesha mchakato wa ajira mara kwa mara.

Tumeweza kutembelea taasisi 18 zilizopo Dar es Salaam na Pwani ili kupata mrejesho wa  wa kazi tunazozifanya na hususan ubora wa Watumishi wanaopangiwa kazi kwenye Mamlaka zao.Taasisi tulizozitembelea ni pamoja na hizi zifuatazo; Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha na Mipango, Maliasili na Utalii, Viwanda Biashara na Uwezeshaji, Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mamlaka ya Hali ya Hewa, Wakala wa Ukaguzi wa Madini, Wakala wa Majengo Tanzania, Wakala wa Serikali Mtandao, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Pwani, Halmashauri za Manispaa ya Ilala,Kinondoni na Temeke na Pia Halmashauri za Wilaya za Bagamoyo na Mkuranga kwa Mkoa wa Pwani. Ziara hizi za tathmini tunatarajia kuziongeza pale bajeti itakaporuhusu. Katika ziara tulizozifanya awali zimetuwezesha kupata ushauri na maoni mengi chanya kwa ajili ya kuboresha utendaji wa taasisi yetu.

Sekretarieti ya Ajira imeweza kushauriana na Waajiri namna bora ya kuhakikisha Watumishi wanaopelekwa kwao wanabaki katika Utumishi wa Umma ili kupunguza wimbi la kuomba vibali vya ajira mara kwa mara. (Retention System). 

Sekretarieti ya Ajira imekuwa ikifuatilia kuona kwamba Watumishi wanaochaguliwa na Sekretarieti ya Ajira ndio hao wanaopewa barua za Ajira na si vinginevyo.

Sekretarieti ya Ajira imeweza kuwa kiungo kati ya Taasisi za Mafunzo, Waajiri na Waombaji kazi Serikalini:

Imeweza kudhibiti taarifa za Waajiriwa kwa kushirikiana na mamlaka za Ajira, Taasisi za umma kama NECTA, na ORMUU, SA imeweka mikakati ya kudhibiti taarifa za waajiriwa ili kuepuka kuajiri watumishi ambao siyo stahili (checks and balances).

Kuimarisha Uzingatiaji wa Ikama katika kuajiri kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Sekretarieti ya Ajira imekuwa na utaratibu wa kuhakikisha mamlaka ya ajira ina kibali cha ajira.Hali hii inadhibiti Mamlaka kutangaza nafasi zilizo nje ya bajeti

CHANGAMOTO

Mheshimiwa Waziri,

Pamoja na kupata mafanikio makubwa ya kiutendaji tangu kuanzishwa kwake Sekretarieti ya Ajira katika utendaji kazi wake inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama ifuatavyo;

Kukuwa kwa teknolojia nchini na duniani kumewafanya baadhi ya wadau kuitumia vibaya mitandao hasa ile ya kijamii hadi  kufikia hatua ya baadhi ya watu kwa utashi wao usiojali maslahi ya Serikali na wananchi wake kuamua kuandaa matangazo ya uongo ya Ajira na kujifanya ni Sekretarieti ya Ajira imetangaza kwa kutumia mitandao ya kijamii na kupotosha Umma.

Ufinyu wa Bajeti na mtiririko mdogo wa fedha kulikopelekea baadhi ya malengo kushindwa kufikiwa ipasavyo kulingana na mahitaji kama yalivyoainishwa katika Mpango Kazi wa mwaka hadi mwaka;Maeneo mengi yaliyoathirika ni yenye kuhitaji mbinu za kisasa za uendeshaji wa michakato ya Ajira.

Mgongano wa kisheria kati ya Sheria iliyoanzisha Sekretarieti ya Ajira na baadhi ya Taasisi za Umma ambazo nazo zina mamlaka kisheria ya kuajiri watumishi kwenye Taasisi zao. Tulishawasilisha mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ambapo mpaka sasa eneo ambalo limeshafanyiwa kazi ni la ugatuaji wa madaraka kwa kukasimisha sehemu ya madaraka.

Uwepo wa baadhi ya waombaji wa kazi kuendelea na kughushi sifa za kielimu na kitaaluma na taarifa binafsi pamoja na hatua kali zinazochukuliwa na Serikali.

Mchakato wa upekuzi wa Maafisa Waandamizi (vetting) kuchukua muda mrefu na hivyo lawama nyingi kuelekezwa kwenye taasisi yetu.

NAMNA TULIVYOTATUA CHANGAMOTO

Mheshimiwa Waziri,

Tumeweza kutatua changamoto zinazotukabili kamaifuatavyo;-

Ufinyu wa Bajeti; Sekretarieti ya Ajira imeweza kuweka   vipaumbele vichache vinavyoweza kutekelezeka ili kuweza kuendana na kiasi kinachopokea, pamoja na kutumia fedha kulingana na malengo iliyojiwekea katika kutekeleza majukumu.

Sekretarieti ya Ajira ingependa kuwa na jengo lake ili kuondokana na gharama za kupanga, hata hivyo, kutokana na ufinyu wa bajeti suala hilo halijaweza kutekelezeka kwa wakati.

Sekretarieti ya Ajira iliandaa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 na Kanuni zake mbapo iliainisha baadhi ya mapungufu ya kisheria na kuyawasilisha kwenye mamlaka husika;

Ofisi inaendelea kutumia rasilimali kidogo inayopata kwa kuhabarisha Umma kuhusu utekelezaji wa Majukumu yake kupitia vyombo mbalimbali pamoja na kutumia fursa mbalimbali ikiwemo kuongea na Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya juu, matumizi ya intaneti na mitandao ya kijamii, mikutano, saili na maonesho mbalimbali ili kuendelea kutoa elimu kwa umma ikiwa ni pamoja na kuanzisha dawati/simu za kiganjani kwa ajili ya kujibu hoja/maswali mbalimbali ya wadau papo hapo ili kukuza uelewa na kuboresha utoaji wa huduma;

Katika kukabiliana na malalamiko ya wadau Ofisi imeendelea kujibu malalamiko hayo kwa njia ya mitandao inayopendelewa sana na waombaji kazi vijana pamoja na kuwa na dawati la kushughulikia malalamiko ambapo Maafisa wawili Waandamizi wanakutana ana kwa ana na wadau na kujibu/kutatua kero zao;

Wale wanaobainika kughushi taarifa mbalimbali wakati wa uendeshaji mchakato wa ajira baada ya kujiridhisha na Mamlaka mbalimbali zenye dhamana ya kutoa sifa au vyeti hivyo wamekuwa wakiondolewa katika mchakato na kukosa fursa ya kupata kazi husika walioiomba;

Ofisi imejipanga kwa kuwa na Mpango wa mafunzo ambao utawezesha kuwa na utaratibu wa kujiendeleza ama kutoa mafunzo   ya pamoja kulingana na hali ya fedha itakavyoruhusu;

Sekretarieti ya Ajira imewasilisha mapendekezo ya kuhuisha Miundo mbalimbali ya Utumishi ili iweze kuendana na mahitaji ya sasa.

MAHUSIANO YA SEKRETARIETI YA AJIRA NA WADAU WAKE

Mheshimiwa Waziri,

Sekretarieti ya Ajira imeweza kuimarisha mahusiano yake na wadau kama ifuatavyo;-

Wizara Mama kwa Sekretarieti ya Ajira

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni taasisi iliyopo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ambayo imekuwa ikitupa ushirikiano wa kutosha kila tulipohitaji ikiwemo Watalaam mbalimbali ambao tumekuwa tukishirikiana nao katika kuendesha usaili.

Taasisi  za Waajiri Serikalini na Wadau wengine.

Mheshimiwa Waziri,

Mchakato wa Ajira hufanywa na Sekretarieti ya Ajira kwa niaba ya Mamlaka za Ajira zifuatazo:

Wizara, Idara Zinazojitegemea na Wakala za Serikali;

Sekretarieti za Mikoa;

Mamlaka za Serikali za Mitaa, na;

Taasisi za Umma.

Kwa kuwa Sheria iliyoanzisha Sekretarieti ya Ajira inataka kuwashirikisha Wataalamu kwenye Mchakato wa Ajira, tumekuwa tukifanya hivyo kwa kuwashirikisha Waajiri kuanzia ngazi ya Shortlisting hadi kwenye Majopo ya usaili.  Ushirikiano huo umeonesha mafanikio makubwa.

Taasisi imeendelea kujifunza kupitia njia mbalimbali ikiwemo kubadilishana uzoefu na taasisi zingine za namna yake zinazojishughulisha na kuendesha michakato ya Ajira nchini. Katika mwaka wa fedha 2016/17, tulibadilishana uzoefu na taasisi binafsi hususan za kimataifa kama Ernest and young, Price Water house Coopers (PWC), shirika la kazi duniani (ILO) na CRDB.

WAJUMBE WA  SEKRETARIETI YA AJIRA

Mheshimiwa Waziri,

Utekelezaji wa majukumu yetu umerahisishwa sana kutokana na Ushirikiano na maelekezo maridhawa ya Wajumbe wa Sekretarieti ya Ajira. Maekezo hayo yanapatikana kupitia vikao vya kawaida ambavyo hufanyika mara nne (4) kwa mwaka au vikao maalum ambavyo hufanyika mara kwa mara kutokana na kazi zinavyojitokeza. Vikao hivyo vya aina mbili hutoa maamuzi katika masuala yafuatayo;

Mpango Mkakati na Mpango Kazi wa mwaka;

Taarifa ya Utekelezaji ya majukumu;

Kupitia na kuidhinisha orodha ya waombaji kazi;

Matokeo ya usaili; na

Masuala mengine yanayohitaji idhini ya Wajumbe wa Sekretarieti.

Mheshimiwa Waziri,

Katika kutekeleza falsafa ya hapa kazi tu, kwa vitendo Bodi ya Wajumbe iliyozinduliwa na aliyekuwa Waziri mwenye dhamana tarehe 5 Oktoba, 2017 ilianza kutekeleza majukumu yake kwa kupata semina pamoja na kuendesha kikao cha kwanza cha Bodi siku ya tarehe 11 Oktoba, 2017 siku sita tu baada ya uzinduzi.

MIPANGO YA BAADAYE

Mheshimiwa Waziri,

Uendeshaji wa Usaili.

Licha ya changamoto hizo, Sekretarieti ya Ajira inatarajia:

Kuendelea kushauri kupitia Ofisi yako juu ya marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma na Sheria nyinginezo zinazohusiana na suala la ajira katika Taasisi mbalimbali za Umma ili ziendane na Sheria ya marekebisho ya Sheria Na. 18 ya mwaka 2007.

Kuwa na mfumo madhubuti wa kielektroniki utakaozungumza na mifumo mingine katika kuendesha mchakato wa ajira ili kuwapata waombaji wenye sifa. Ili kufanikisha dhamira hiyo tupo kwenye mazungumzo na baadhi ya Taasisi zikiwemo OR-MUUB, TCU, NECTA, NIDA.

Kupunguza gharama za matangazo na muda wa kuendesha mchakato wa Ajira kwa kutumia zaidi Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Kuendelea kuwa na ushirikiano na wataalam toka Taasisi mbalimbali pamoja na waajiri ili kuwapata waombaji wenye sifa.

Uwezo wa Taasisi kutekeleza Majukumu yake

Mheshimiwa Waziri,

Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ina jumla ya Watumishi 73. Idadi hii ni pungufu ya watumishi 13 ikilinganishwa na ikama ya Watumishi 86 iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Kati ya Watumishi 73 waliopo, Wataalamu ni 49 na 25 ni “Supporting Staff”.

TAALUMA

Watumishi wana sifa na taaluma zinazohitajika katika kutekeleza majukumu yao. Hata hivyo, kutokana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika kutekeleza majukumu yao wanahitaji kujengewa uwezo zaidi kitaaluma. Watumishi watano (5) wanaendelea na mafunzo ya muda mrefu ya shahada ya uzamili katika fani za TEHAMA (1) na Rasilimali Watu (4). Kati ya watumishi hao watano (5) watumishi wawili (2) wanahudhuria mafunzo kwa ufadhili wa Serikali na Watatu wanafadhiliwa na wadau wa maendeleo (Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China)  Lengo ni kuwajengea uwezo wa kitaaluma Watumishi tulionao ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wao. Taasisi itaendelea kuwajengea uwezo Watumishi wake pale uwezo wa kibajeti utakapo ruhusu.

HITIMISHO

Mheshimiwa Waziri,

Ili chombo hiki kiweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi haina budi kuwezeshwa hasa katika eneo la rasilimali fedha, kwa kupata bajeti inayokidhi mahitaji. Pale ambapo chombo hiki kitapata rasilimali fedha ya kutosheleza kutaifanya Sekretarieti ya Ajira iweze kuongeza weledi kwenye kazi zaidi pamoja na kutumia mbinu za kisasa kwenye mifumo yake. Kupitia mifumo mipya na ya kisasa, nchi yetu na waajiri watapata rasilimali watu waliokidhi mahitaji ya sasa.

Naomba nikuhakikishie kuwa Sekretarieti ya Ajira itaendelea kutekeleza jukumu la kuendesha mchakato wa Ajira kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu pamoja na miongozo mbalimbali ikiwa pamoja na kuzingatia yale tuliyoyaahidi kwenye Mkataba wetu kwa Mteja. Pamoja na kutekeleza maelekezo yako yatakayotolewa mara kwa mara kwa mujibu wa Sheria.

Mheshimiwa Waziri,

Baada ya kusema haya naamini hadhara hii ni yako, kwa kuwa jukumu langu lilikuwa kueleza majukumu yetu kwa ufupi na nini tumeshafanya, hivyo, kwa Niaba ya Menejimenti na Watumishi wote wa Sekretarieti ya Ajira nikukaribishe tena kwa mara nyingine katika ofisi yako hii ili uweze kutupa nasaha zako.

Mwisho, nikamkaribishe Katibu Mkuu, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Laurian Ndumbaro ili aweze kutoa neno na kukukaribisha wewe.

Naomba kuwasilisha na ahsanteni kwa kunisikiliza.