Call for Interview

Placements

Visitors Counter

»Today   1440               
»Week   1440               
»Month   29201               
==============
»Total  23379587        

Sekretarieti ya Ajira yakutana na Wanafunzi wa Chuo cha Madini

July 4, 2018


Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetoa elimu ya masuala mbalimbali kuhusu mchakato wa ajira serikalini katika Chuo  cha Madini Dodoma ikiwa ni hatua endelevu ya utekelezaji wa mkakati wake wa kutatua changamoto  mbalimbali ambazo zimekuwa zikibainika wakati wa utekelezaji wa mchakato wa Ajira Serikalini kwa kukutana na wadau wake ikiwemo wanafunzi wa Vyuo mbalimbali nchini.

Katika maadhimisho ya siku ya Madini Duniani iliyofanyika chuoni hapo mwishoni mwa wiki mada mbalimbali zilitolewa  kwa Wanafunzi wa Chuo hicho ambapo miongoni mwa mada zilizotolewa ni kuhusu  matumizi ya TEHAMA katika mfumo wa kujisajili wakati wa kuwasilisha maombi ya kazi (Recruitment Portal), pamoja na masharti ya msingi ya kuzingatia kabla na baada ya kuwasilisha maombi ya kazi.

Afisa Mawasiliano kutoka Sekretarieti hiyo Bw. Kassim Nyaki akiongea na wanafunzi wa chuo hicho alibainisha kuwa mada hizo zimelenga kutatua changamoto pamoja na kutoa uelewa kwa wanafunzi wa Vyuo ili watakapohitimu waweze kujua majukumu ya Sekretarieti ya Ajira, taratibu za kufuata kabla ya kuomba ajira Serikalini, namna ya kujiandaa kabla na wakati wa usaili pamoja na utaratibu wa uwasilishaji wa maombi ya kazi kwa njia ya mtandao ujulikanao kama Recruitment portal.

“Sekretarieti ya Ajira tunatambua kuwa wahitimu wa vyuo ni sehemu ya wadau wetu wakubwa katika kutekeleza Mchakato wa Ajira serikalini, na tunatambua kuwa baada ya kuhitimu masomo baadhi yenu mmejipanga kuingia katika soko la ajira ambalo linahitaji watu wenye sifa, weledi na maadili mema ili kuisaidia Serikali kufikia malengo yake.” alisisitiza Nyaki.

Aliongeza kuwa, Sekretarieti ya Ajira katika kukabiliana na changamoto inazokumbana nazo wakati wa uendeshaji wa mchakato wa Ajira imeamua kuwa na mkakati wa kuwafuata wadau wake kuzungumza, kuwaelimisha  pamoja na kupata mrejesho kutoka kwao ili wanapoanza kuwasilisha maombi ya kazi kupitia Sekretarieti hiyo  wawe na uelewa  wa kutosha kuhusu taratibu za kuomba kazi, namna ya kuandaa wasifu binafsi (CV) namna ya kuandika  barua za maombi ya kazi, jinsi ya kujiandaa kabla na wakati wa usaili ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuweza kushindana katika soko la ajira nchini.

Bi. Mtage Ugullum ambae ni Afisa TEHAMA kutoka Sekretarieti ya Ajira nae alitumia fursa hiyo kutoa elimu kwa vitendo kwa Wanafunzi hao kuhusu namna ya kujiunga katika Mfumo wa maombi ya kazi kupitia ‘Recruitment Portal’.

Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Chuo hicho anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri Bw. Fredrick M. Mangasini amewashauri wanafunzi wa Chuo hao kutumia fursa hiyo kujifunza kwa makini huku wakitambua kwamba soko la Ajira lina ushindani mkubwa kutokana na kuwa wahitimu ni wengi hivyo ni vyema wakajiandaa kisaikolojia ili kuweza kushindana katika soko hilo na kupata fursa ya kuajiriwa Serikalini.    

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.