Call for Interview

Placements

Visitors Counter

»Today   1443               
»Week   1443               
»Month   29204               
==============
»Total  23379590        

Vigezo ndio sharti muhimu la kupata Ajira Serikalini

June 22, 2018


Wadau wa Sekretarieti ya Ajira wametakiwa kutambua kuwa ili kupata Ajira katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinachozingatiwa ni sifa  za mwombaji na masharti yaliyobainishwa katika tangazo la nafasi ya kazi husika na si vinginevyo.

Katibu wa Sekretarieti ya Ajira Bw. Xavier Daudi amebainisha hayo leo alipokuwa akiongea na baadhi ya wadau waliotembelea Ofisi za Taasisi hiyo zilizopo eneo la Shangani Zanzibar wakitaka kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu utaratibu wa Ajira Serikalini, ambapo  Sekretarieti ya Ajira inaendelea kutoa huduma kwa wadau wake kwa upande  wa Zanzibar na Dar es salaam katika kipindi hiki cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo yameanza tangu tarehe  16 Juni, 2018 na yanatarajiwa kumalizika tarehe 23 Juni mwaka huu.

"Ni vizuri mkafahamu kuwa fursa zote za Ajira katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinatolewa kwa kuzingatia sifa za mwombaji, masharti ya nafasi ya kazi inayotangazwa, haya mnayoyasikia sijui upendeleo, rushwa au vimemo hakuna kitu kama hicho kutokana na mifumo yetu tuliojiwekea” alisema Daudi.

Sambamba na hilo amewataka wadau hao kutambua kuwa kwa sasa wahitimu ni wengi  hali ambayo imeongeza ushindani ili mtu aweze kupata kazi ni lazima awe amejiandaa vizuri kuanzia akiwa masomoni, awe ni mtu mwenye maadili mema kwa kuwa Serikali ina malengo iliyojiwekea na ili yaweze kufikiwa ni lazima ipate mtu mwenye maadili mema ambaye anaweza kutekeleza majukumu yake kwa wakati.

Aidha, alibainisha kuwa baadhi ya changamoto ambazo Ofisi yake inakumbana nazo ni pamoja na baadhi ya wahitimu kukosa ubora unaendana na taaluma waliyonayo, kudanganya sifa, kutozingatia vigezo vinavyotolewa kwenye tangazo wakati wa kuwasilisha maombi pamoja na mmomonyoko wa maadili.